YouVersion Logo
Search Icon

Mwanzo 27:18-29

Mwanzo 27:18-29 BHN

Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?” Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.” Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.” Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.” Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.” Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki. Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.” Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa. Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.” Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema, “Tazama, harufu nzuri ya mwanangu ni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu! Mungu akumiminie umande wa mbinguni; akupe ardhi yenye rutuba, nafaka na divai kwa wingi. Jamii za watu zikutumikie, na mataifa yakuinamie kwa heshima. Uwe mtawala wa ndugu zako, watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima. Kila akulaaniye na alaaniwe, kila akubarikiye na abarikiwe!”

YouVersion uses cookies to personalize your experience. By using our website, you accept our use of cookies as described in our Privacy Policy